Je, wewe ni mwenye nyumba uliyepokea msaada wa FEMA kwa ajili ya matengenezo ya nyumba yako? Je, baadaye uligundua kwamba tanuri lako liliharibiwa au kubomolewa na Kimbunga Ida?
Ikiwa tanuri lako halikuwa limekatiwa bima, FEMA wanaweza kukupa ufadhili wa ziada kutengeneza au kupata tanuri jipya. Lakini ni sharti ukate rufaa kwa FEMA kwa maandishi na uambatishe risiti za kuthibitisha matengenezo au makadirio ya gharama.
FEMA wanaweza kufidia hadi kufikia gharama iliyoandikwa kwenye risiti au makadirio ya tanuri jipya. Ikiwa ulitengeneza au kubadilisha tanuri, FEMA wanaweza kutoa msaada wakati makadirio au risiti halali zitatolewa kwenye rufaa. Unapotuma maombi ya msaada, hakikisha kwamba umetoa taaarifa za uharibifu wa tanuri uliotokana na Kimbunga Ida.
Ufadhili utatolewa kwa waathiriwa stahiki katika kaunti za Bronx, Kings, Nassau, Queens, Richmond, Rockland, Suffolk, na Westchester, ambazo zilijumuishwa kwenye tangazo la taifa kuhusu Kimbunga Ida. Makazi yatakayofadhiliwa ni yale ya msingi yanayokaliwa na wamiliki. Makao ya likizo na makao ya ziada hayatafadhiliwa.
Ufadhili wa Matengenezo ya Makao unatolewa tu kwa wenye nyumba ambao hawakuwa na bima ya makao yao au waliokuwa na bima ndogo kuliko thamani ya mali yao na kwa gharama zinayohusiana na mkasa zinazolenga kuyafanya makao yawe salama, safi na bora. Ufadhili mwingine wa FEMA pia unapatikana kugharamia vipengele vingine vya kimuundo katika makao yako ya msingi ikiwemo visima, mfumo wa maji taka, mfumo wa maji moto na vyombo vingine vya kielektroniki.
Kumbuka: Lazima utume maombi ya rufaa kwa maandishi ndani ya siku 60 kuanzia tarehe iliyo kwenye barua ya maamuzi ya FEMA. Kumbuka kuambatisha stakabadhi za ithibati kuyapa uzito maombi yako ya rufaa kama vile risiti halali za matengenezo au makadirio yake, makadirio ya mafundi au ushahidi mwingine kuipa rufaa yako uzito.
Baada ya kutuma rufaa yako kwa FEMA, utarajie barua ya maamuzi ndani ya siku 90 baada ya kupokelewa kwa barua yako na FEMA.
Ukiwa na maswali kuhusu namna ya kutuma rufaa yako, tembelea Kituo Cha Kutoa Misaada ya Mikasa– DRC Locator (fema.gov) – au piga Simu ya FEMA ya Usaidizi kupitia 800-621-3362. Ikiwa unatumia nambari au laini ya simu ya wasiosikia/walemavu (relay call) kama vile huduma ya relay ya video, huduma ya simu ya maandishi (captioned telephone) au huduma nyingine, wape FEMA nambari ya huduma hiyo. Wahudumu katika laini za usaidizi wanapatikana kuanzia saa mbili asubuhi (8 a.m.) hadi saa moja jioni (7 p.m.) kila siku. Bonyeza 2 kupata huduma kwa lugha ya Kihispania au 3 kupata mkalimani anayezungumza lugha yako.
Kutuma maombi ya msaada wa FEMA, unaweza pia kupiga Simu ya FEMA ya Usaidizi, kutembelea DisasterAssistance.gov au utumie app ya simu ya FEMA.
Watu wa kipato cha chini wanaokabiliwa na masuala ya kisheria yaliyotokana na Kimbunga Ida wanaweza kupiga simu isiyokuwa na malipo kupitia 888-399-5459 ili kupata ushauri. Ikiwa unahitaji mtoa huduma ya kisheria awasiliane nawe, Unashauriwa kujaza fomu kupitia https://nysba.org/ida. Mifano ya usaidizi wa kisheria unaopatikana ni pamoja na:
- ushauri nasaha kuhusu masuala ya mpangangaji na mwenye nyumba
- usaidizi kushughulikia mikataba ya ukarabati wa nyumba na ya mafundi
- masuala ya kumlinda mteja kama vile kupandishwa bei za vitu na kuepuka ulaghai wa mafundi katika mchakato wa kujenga upya
- usaidizi wa kupata mafao ya serikali
- usaidizi wa madai ya bima ya maisha, afya, na mali
- ushauri nasaha kuhusu matatizo ya mkopo wa nyumba
Kupata habari zaidi mtandaoni pamoja na vijitabu vya FEMA vinavyoweza kupakuliwa, tembelea DisasterAssistance.gov kisha ubofye “Information.”
Kwa rufaa kwenda kwa mashirika yanayosaidia katika mahitaji mahususi ya jamii, piga simu 211 au temebelea https://www.211nys.org/contact-us. Kwa wakazi wa mji wa York City, piga simu 311.
Kwa taarifa za hivi karibuni kuhusu juhudi za kutoa misaada kwa waathiriwa wa Kimbunga Ida, tembelea fema.gov/disaster/4615. Fuatilia taarifa zetu kwenye kurasa zetu za mitandao ya kijamii kupitia twitter.com/femaregion2 na facebook.com/fema.