Kuvu: Matatizo na Suluhisho

Release Date:
Julai 29, 2023

Ikiwa nyumba yako ilipata mafuriko, kuvu inaweza kuwepo na inaweza kusababisha hatari ya afya. Unaweza kuona au kunusa kuvu kwenye nguo, ukuta au fanicha, na inaweza kufichwa chini au nyuma ya vitu kama sakafu, vifaa au kuta. Kukausha nyumba yako na kuondoa vitu vilivyoharibiwa na maji ni hatua muhimu zaidi ya kurekebisha uharibifu wa kuvu.

Kuvu inaweza kusababisha:

  • Hatari za kiafya: Viiniyoga vya kuvu ni viumbe vidogo vidogo ambavyo huelea angani na kusababisha matatizo ya mizio, pumu, maambukizi na masuala mengine ya kupumua. Kuvu inaweza kusababisha matatizo ya matibabu kwa mtu yeyote - lakini watoto wachanga, watoto, wazee, na wale walio na kinga dhaifu wanaweza kupata athari kali zaidi. Watu wenye matatizo ya kupumua kama vile pumu au mfumo dhaifu wa kinga wanapaswa kukaa mbali na ukungu.
  • Uharibifu wa jengo: Inawezekana kuwa na uharibifu wa kuvu hata kama huna uharibifu mwingine unaoonekana. Ikiwa nyumba yako ina kuvu, kila kitu kilichoathiriwa lazima kisafishwe na kukaushwa. Bidhaa ambazo haziwezi kusafishwa vizuri na kukaushwa ndani ya masaa 24-48 lazima zitupwe, ikiwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi na mali ya kibinafsi. Watoto hawapaswi kushiriki katika kazi ya kusafisha baada ya majanga.

Jinsi ya Kuondoa Kuvu

Kuondoa kuvu na kurekebisha nyumba inaweza kuwa kazi ngumu au hatari, kwa hivyo inaweza kuwa bora kupata msaada kutoka kwa mtaalamu. Ikiwa ni lazima uondoe kuvu mwenyewe, fuata hatua hizi:

  • Vifaa vya Kujikinga: barakoa au miwani ya macho, barakoa ya kukinga uso (kama vile kipumulio cha N95), glavu, shati la mikono mirefu, suruali ndefu na buti ambazo haziingizi maji zitakusaidia kuepuka kugusa kuvu.
  • Kausha Jengo: Safisha na ukaushe jengo haraka iwezekanavyo. Ikiwa nyumba yako imekuwa tupu kwa siku kadhaa, fungua milango na madirisha ili kuruhusu hewa kutoka kwa nyumba kwa angalau dakika 30 kabla ya kukaa kwa muda mrefu. Fungua milango ya ndani, haswa makabati na vyumba vya ndani. Fungua kabati za jikoni na milango ya bafuni, na uipanguze kwa sabuni na maji. Wakati umeme ni salama kutumia, tumia feni na viondoa unyevu kusambaza hewa na kuondoa unyevu. Weka feni ili kupuliza hewa nje ya milango na madirisha. Angalia mfumo wako wa kuongeza joto, uingizaji hewa na viyoyozi kabla ya kuuwasha ili usieneze ukungu kwenye nyumba yako.
  • Ondoa Vifaa vyote Vilivyoathiriwa: Ondoa na utupe chochote kilichokuwa na unyevu na kisichoweza kusafishwa na kukaushwa kabisa.
  • Safisha: Safisha kwa sabuni na maji. Ondoa kuvu yote unayoweza kuona. Kausha mara moja. Usichanganye bidhaa za kusafisha. USICHANGANYE dawa ya klorini (bleach) na amonia - kufanya hivyo kutatengeneza mivuke yenye sumu. Baada ya kumaliza kusafisha nyumba, oga na ubadilishe nguo zako haraka iwezekanavyo ili kuzuia kupeleka kuvu kwenye nyumba yako ya sasa ya kuishi.
  • Jitayarishe Kurekebisha: Kupaka rangi au kufunika kuvu hakutaizuia kukua. Rekebisha tatizo la maji au unyevu kabisa na safisha kuvu yote kabla ya kupaka rangi. Ondoa kuvu yote na kuua vijidudu kila mahali kuvu ilikuwepo kabla ya kuanza ukarabati. 

Tuma Maombi ya Msaada wa FEMA

Ikiwezekana, piga picha za uharibifu kabla ya kurekebisha nyumba yako. Weka risiti za gharama zote za kurekebisha ulizolipia mwenyewe ili kuonyesha mkaguzi wa FEMA - hii itahakikisha kuwa wana rekodi sahihi zaidi ya uharibifu na gharama zako kwa ripoti yao.

Ili kutuma ombi la msaada wa FEMA, piga simu kwa laini ya msaada 800-621-3362, tembelea DisasterAssistance.gov au pakua FEMA App. Ikiwa unatumia huduma ya usambazaji kama vile huduma ya usambazaji video (VRS), huduma ya simu iliyo na maelezo mafupi au nyinginezo, pea FEMA nambari yako ya huduma hiyo unapotuma ombi. 

Kupata msaada ana kwa ana, tembelea Kituo cha Msaada wa Majanga, ambapo wataalamu wa FEMA wanaweza kusaidia katika kutuma maombi, kujibu maswali na kutoa marejeleo ya rasilimali. Ili kupata kituo karibu nawe, tembelea fema.gov/drc.

FEMA imejitolea kuhakikisha usaidizi wa majanga unatekelezwa kwa usawa, bila ubaguzi kwa misingi ya rangi, dini, utaifa, jinsia, umri, ulemavu, ujuzi wa Kiingereza, au hali ya kiuchumi. Mwathiriwa yeyote wa majanga au mwananchi anaweza kuwasiliana na Ofisi ya Haki za Kiraia ya FEMA ikiwa anahisi kuwa ameathiriwa na ubaguzi. Ofisi ya Haki za Kiraia ya FEMA inaweza kupatikana bila malipo kwa 833-285-7448. Maopareta wanaotumia lugha mbali mbali wanapatikana.

Tags:
Ilisasishwa mara ya mwisho